HATUKUKUBALIANA! KIZAZAA HUKU WAMILIKI WA MATATU WAKITOFAUTIANA NA WAZIRI WANDAYI KUHUSU MAZUNGUMZO YA BEI YA MAFUTA.
Written by Ushindi Winsky on May 19, 2026
Picha ya pamoja ya mdau wa usafiri na Waziri wa Nishati wakati wa mkutano na wanahabari katika jengo la Transcom House mnamo Mei 18, 2026.Hali ya wasiwasi ilitokea katika mkutano wa moja kwa moja jengo la Transcom siku ya Jumatatu baada ya wawakilishi wa sekta ya matatu kukataa hadharani kauli ya Waziri wa Nishati, Opiyo Wandayi. Walisisitiza kuwa hakuna makubaliano yoyote yaliyofikiwa kuhusu mabadiliko ya bei ya mafuta.
Akizungumza kwenye mkutano huo, Opiyo Wandayi alisema serikali inakusudia kupunguza tofauti ya bei kati ya dizeli na petroli. Alisema lengo ni kuzuia uchakachuaji wa mafuta na kulinda magari yanayotumia dizeli yasiharibike.“Ili kuondoa hatari ya kuchakachua mafuta kwa sababu ya tofauti hii kubwa ya bei,” Wandayi alisema, “tutapunguza mwanya uliopo kati ya bei ya dizeli na petroli.”
Waziri alieleza kuwa katika mpango huo, bei ya dizeli itapunguzwa huku bei ya mafuta ya taa ikiongezwa ili kuleta usawa wa bei.Aliongeza kuwa mazungumzo hayo yalifanywa pamoja na Mamlaka ya Kudhibiti Nishati na Petroli (EPRA), na kwamba maelezo kamili yatatolewa rasmi na mamlaka hiyo.“Lazima niongeze kuwa EPRA ilihusika kikamilifu, na uelewa huu umefikiwa na pande zote kwa kauli moja,” alisema Wandayi.Hata hivyo, muda mfupi baadaye, wawakilishi wa sekta ya usafiri walimpinga Waziri huyo vikali. Walitangaza kuwa hakuna mwafaka uliopatikana na kwamba mazungumzo bado hayajakamilika.“Kuna mambo ambayo hatukubaliani hapa,” alisema mwakilishi mmoja, akisisitiza kuwa umma unapaswa kujua kuwa wahudumu wa matatu hawajaunga mkono pendekezo la serikali.
Mwakilishi huyo aliongeza kuwa wahudumu walikuwa wamependekeza bei tofauti ya kati ya Sh30 na Sh35. Aliishutumu serikali kwa kutangaza makubaliano ambayo hayapo.“Hatukukubaliana kuhusu jambo lolote,” alisema. “Hicho ndicho tunataka wanachama wetu na taifa nzima wajue.”Matamshi hayo yalimalizika kwa kuthibitisha kuwa mgomo uliopangwa bado upo palepale.
Hii inaashiria uwezekano wa kuvurugika kwa usafiri nchini ikiwa mazungumzo mapya hayatatua mzozo huo.Kutofautiana huku kunaonyesha mvutano unaoongezeka kati ya serikali na wahudumu wa usafiri wa umma, wakati ambapo Wakenya wengi tayari wanahangaika na gharama kubwa ya maisha na nauli kupanda.
