USIWE KITATANGE KUWATOSA WENZAKO DEMANI:
Written by Daniel Masese on September 4, 2024
Jumatano,4.Septemba.2024.
USIWE KITATANGE KUWATOSA WENZAKO DEMANI:
Usiwe kitatange kuwatosa wenzako demani:
Katika barabara barabara za bara na za maisha,
Ongoza kwa ujasiri, umahiri wala si kwa usiri.
Usiwe kivuli kilichozisheheni tumbi tumbi shari,
Upotofu, upotovu nao utindikiwa.
Aangukapo shimoni gizani totoro, mpe kamba.
Falsafa za huyu ni mnyonge, mnyonge, zisikupoteze.
Usiwe mikatale ya ukale butu isiyo nayo makali.
Usiwe kitatange kuwatosa wenzako demani.
Usiwe kitatange kuwatosa wenzako demani,
Heshima, busara, fikra, fakra, sura pamwe nazo sera
Maridhawa zako hewani zisiyalete machafuko nayo
Mazingara katika mazingira.
Usiwe kitatange kuwatosa wenzako demani.
Usiwe kitatange kuwatosa wenzako demani,
Uongozi ni ujenzi, ujuzi usio wa juzi.
Usiyazalishe makenya; usivikuze, usivitunze na
Usivituze virugu na kuyakopoa makovu mitimani mwao.
Uzihalalishe halali, uziharamishe haramu.
Mla kuku humlipa tembo babu kubwa.
Malango ya fursa nazo satua uwafungulie.
Mwangaza wa mafanikio uwe ndio mkongojo wako.
Usiwe kitatange kuwatosa wenzako demani.
Shukran jazzilan.
Fiamanillah.
Masalaam.
Naye: Fanani, Mbega, Mbuji, Mbuni, Mlimbwende, Mnyange, Mstahiki, Mwanafalsafa na Ustadh Danieli Masese.