Kenya yaimarisha ulinzi mipakani huku maambukizi yakiongezeka DRC na UGANDA
Written by Ushindi Winsky on May 18, 2026
Mhudumu wa afya akipulizia dawa ya kuua vijidudu katika kituo cha matibabu ya Ebola kwenye eneo la afya la Bulape, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), Oktoba 17, 2025. (Shirika la Afya Duniani/Handout kupitia Xinhua). Serikali imezielekeza serikali zote za kaunti kuimarisha mara moja hatua za ufuatiliaji na maandalizi ya dharura kufuatia mlipuko uliothibitishwa wa Ugonjwa wa Virusi vya Ebola (EVD) katika sehemu ya mashariki ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) na kisa kimoja kilichotokea nchi jirani ya Uganda.Katika taarifa yake mnamo Jumamosi, Katibu Mkuu (PS) wa Afya Mary Muthoni alizitahadharisha kaunti kuamsha mifumo ya majibu ya haraka kufuatia kuongezeka kwa harakati za watu na bidhaa katika kanda hiyo. Kulingana na Wizara ya Afya, mlipuko huo katika Mkoa wa Ituri mashariki mwa DRC kufikia sasa umerekodi visa 246 vinavyoshukiwa na vifo 65, vimeripotiwa . Uchunguzi wa kimaabara uliofanywa na mjini Kinshasa ulithibitisha maambukizi ya Ebola katika sampuli 13 kati ya 20 zilizofanyiwa majaribio.PS alibainisha kuwa Uganda ilithibitisha kisa kilichoingia nchini humo kikimhusisha raia wa Kongo mwenye umri wa miaka 59 aliyesafiri kutoka DRC hadi Kampala kutafuta matibabu. Mgonjwa huyo alilazwa katika Hospitali ya Kibuli Muslim mnamo Mei 11 na baadaye akafariki Mei 14 akiwa anapata matibabu. Katika waraka uliotumwa kwa Wanachama wa Kamati Kuu ya Kaunti wa Afya, Wakurugenzi wa Afya wa Kaunti, Maafisa Wakuu wa Afya, na Katibu Mkuu wa Afya ya Jamii, PS Muthoni aliwahakikishia Wakenya kuwa hakuna kisa cha Ebola kilichoripotiwa nchini kufikia sasa.”Wizara ya Afya inapenda kuwahakikishia Wakenya wote kuwa, hadi leo, hakuna kisa kilichothibitishwa au kinachoshukiwa cha ugonjwa wa virusi vya Ebola ambacho kimegunduliwa ndani ya Jamhuri ya Kenya,” PS alisema. “Hata hivyo, kutokana na harakati kubwa za watu na bidhaa ndani ya kanda ya Afrika Mashariki na Kati, Serikali zote za Kaunti zinaelekezwa kuamsha na kuimarisha mara moja hatua za maandalizi na majibu.” PS alizielekeza kaunti kuimarisha ukaguzi na ufuatiliaji katika viwanja vya ndege, nyanja ndogo za ndege, bandari, vituo vya mipakani na maeneo ya kupitishia wasafiri.Serikali za kaunti pia zilielekezwa kuimarisha mifumo ya ufuatiliaji katika ngazi ya jamii ili kurahisisha ugunduzi wa mapema na utoaji wa taarifa za visa vinavyoshukiwa. PS Muthoni alitoa wito wa kuamshwa kwa Vikundi vya Majibu ya Haraka vya Kaunti na Vituo vya Operesheni za Dharura za Kaunti ili kuhakikisha uchunguzi wa haraka na udhibiti wa maambukizi yoyote yanayoshukiwa. Alisema kaunti lazima pia ziimarishe hatua za kuzuia na kudhibiti maambukizi kwa kuhakikisha usambazaji wa kutosha na matumizi sahihi ya vifaa vya kinga binafsi
katika vituo vyote vya afya.”Imarisheni mifumo ya kuchagua wagonjwa ukaguzi, utengaji (isolation), na rufaa katika vituo vyote vya afya,” PS alieleza. Wizara hiyo pia ilizielekeza kaunti kuongeza kampeni za uhamasishaji wa umma kuhusu dalili za Ebola, kinga na mifumo ya kutoa taarifa huku ikipambana na taarifa potofu na hofu. Wahudumu wa afya kote nchini pia wanatarajiwa kupata mafunzo ya kurejelea maarifa kuhusu utambuzi wa visa vya Ebola, usimamizi wa wagonjwa, kuzuia maambukizi na taratibu za mazishi salama.Ugonjwa wa Virusi vya Ebola ni ugonjwa mbaya wa virusi unaoenea kupitia mguso wa moja kwa moja na majimaji ya mwili ya mtu aliyeambukizwa, vifaa vilivyochafuliwa au wanyama wa porini walioambukizwa. Dalili za kawaida ni pamoja na homa kali, uchovu, maumivu ya kichwa, maumivu ya misuli, kutapika, kuhara, maumivu ya tumbo na kuvuja damu au michubuko isiyoelezeka.
Swali ni je! Ni vipi tunaeza jikinga kama wanaanchi wa Kenya ili tuepuke na ugonjwa huu?
